Saturday, June 30, 2012

Exclusive uchambuzi: Wazazi wa Dogo Janja fuatilieni maendeleo yake, msiwaachie Mapromota

Dogo Janja
Na Dotto Kahindi-Thisday Magazine, Blog za mikoa

Mwezi Juni mwaka huu umekuwa ni mwezi wa huzuni na furaha kwa nyota wa muziki wa Bongo Fleva , Abdul Abubakar Chande ‘Dogo Janja’ kufuatia kutimuliwa na Baba yake kimziki Madee na baada ya siku chache kurejea Dar es Salaam na kuingia mkataba mpya na kampuni ya Mtanashati Entertainments.
Dogo Janja alitimuliwa na Madee na kurejeshwa kwao jijini Arusha kwa madai ya kushindwa kuzingatia masomo kwa kuendekeza utoro shuleni, kukosa mwenendo mwema kimaadili sababu ambazo hata hivyo Dogo Janja alizikanusha na kudai kuwa alikuwa akinyanyaswa na Madee.
Alidai kuwa akiwa chini ya usimamizi wa Madee alikuwa akilipwa posho kidogo baada ya kufanya maonyesho na kwamba Madee alihusika kumwibia pesa zake benki hali iliyomfanya kuwa na salio la Tsh.25, 000 elfu tu katika akaunti yake.
Hali ilikuwa hivyo na imeleta picha mbaya na kuibua maswali mengi kwa mashabiki wa muziki lakini lawama kubwa zinafaa kupelekwa kwa wazazi wa Dogo Janja ambao walimruhusu kwa moyo mweupe aje kuishi na watu ambao leo hii wanaonekana kuwa ni wahuni.
Pamoja na kutimuliwa na Madee lakini sasa sasa amerejea tena akiwa katika mwonekano mwingine, naamini muda mfupi aliokaa na wazazi wake walifanya mazungumzo ya kutosha na kufanya makubaliano ya nini kipewe kipaumbela katika maisha yake kwa sasa, ili kumjengea mafanikio yake kielimu na kimaisha pia.
Furaha aliyoipata baada ya kutua Bongo na kujiunga na kampuni ya Mtanashati Entertainments ya jijini Dar es Salaam, zisimfanye akajisahau tena na kuendeleza upuuzi alioufanya akiwa na Madee.
Tukubaliane wote kuwa Dogo Janja bado ni mtoto na anahitaji kupata mwongozo wa kutosha kutoka hasa kwa wazazi wake na watu walio juu ya uwezo wake ili kumsaidia kufanya kila hatua kwa usahihi asije kujuta baadaye.
Pengine kwa hatua ya nyota huyo cha kwenda kusomewa kisomo maalumu cha kuomba Mwenyezi Mungu amnyooshee mambo yake pindi atakapoanza kushusha ngoma mpya kinaweza kuonyesha kuwa kuna nia njema kwa watu alionao sasa.
Maneno ya Mkurugenzi wa kampuni hiyo Ostaz Juma na Musoma kuwa wameamua kumfanyia kisomo hicho kwa lengo la kuweka kazi zote za Dogo janja mikononi mwa Mungu ili kumkinga na watu wabaya ambao kwa namna moja ama nyingine hawajafurahishwa na mpango mzima wa dogo huyo kurejea Bongo.
Hata hivyo katika kipindi kifupi alichojiunga na kampuni hiyo Dogo janja amefanyiwa ‘shopingi’ ya nguvu kwenye maduka makubwa ya viwalo yaliyopo Mlimani City jijini Dar ambayo ilitumia zaidi ya shilingi Milioni 2.5.
Hivi ni miongoni mwa vitu vinavyomfanya Dogo Janja afurahie kuwa katika kampuni hiyo lakini lazima ajue kuwa nidhamu ya kazi ndiyo itamfanya aendelee kupata matunda hayo maana akiendelea kujifanya nunda na kupuuza ya wakubwa wake haitamsaidia.

0 comments:

Post a Comment