Wednesday, July 2, 2014

Professor J aongea na COSOTA kuhusu utaratibu wa Radio na TV kuwalipa wasanii kwa kucheza kazi zao

Msanii wa Hip Hop, Joseph Haule aka Professor J jana amekitembelea chama cha haki miliki Tanzania, ‘COSOTA’ na kuwauliza kwanini Radio na TV za Tanzania haziwalipi wasanii pindi wanapoziga nyimbo zao kwenye vituo vyao.
Professor-Jay1-copy-800x596
Professor ameiambia Bongo5 kuwa baada ya kupeleka shauri hilo, wahusika ambao ni COSOTA wamesema bado wapo kwenye vikao kujadili suala hilo.

“COSOTA sio watu wa mwisho, wameniambia kuna vikao vingine vinaendelea, tuweke subira lakini hili suala linajadiliwa kila siku. Budget ya serikali imepita hakuna kilichoendelea, kama ni matatizo yapo kwenye sheria kwanini isirekebishwe? Lakini tuseme kweli haya mambo yanatakiwa yaanze ingawa kumekuwa na changamoto. Hata wasanii wenyewe wanafanya muziki kama muziki ilimradi wanajifurahisha, lakini kama watakuwa serious vyombo vya habari ‘Radio na TV’ kwa kuwalipa wasanii, maana yake hata wasanii wenyewe watakuwa serious kufanya muziki kwa perfect na itachuja upi mchele zipi pumba, naamini hivyo,” amesema.


“Vyombo vya habari haviwezi kukubali kumlipa mtu ambaye yupo shaghalabaghala ambao hawafanyi muziki ambao unaeleweka. Kenya wenzetu wanalipwa, nimekuawa nikishauriana na wasanii wa Kenya kuhusu hili suala, wakaniambia Kenya kuna baadhi ya wasanii ambao wapo kwenye COSOTA yao, kwahiyo inakuwa ni rahisi wenyewe kuangalia ni jinsi gani wasanii wao wananufaika na muziki wao. Kwetu hapa hili swala likipita kwanza wasanii watanufaika na kazi zao pamoja na serikali itanufaika, pia Radio na TV wakitaka wanufaike na muziki wa wasanii watadili na matangazo, sio kama sasa hivi, TV na Radio zinaingiza pesa nyingi kwa matangazo kutokana na kupiga nyimbo zao kwenye vipindi vyao,” aliongeza.

Professor amewataka wasanii wengine kuungana katika kulifuatilia suala hilo.
“Kinachoonekana kwa wasanii wengi wa Bongo tunaogopa kumfunga Paka kengele, wengi tunaogopa wakati muziki ndo wenye manufaa kwetu. Sasa hivi na baadaye, wazee wetu akina mzee Marijani, Remmy Ongara mwenyezi Mungu amlaze mahali pema, wao tayari wakati wao umepita, sasa hivi ni jukumu letu kuutoa muziki hapa ulipo na kuupeleka kwenye next level na kuwafanya watu wote waweze kunufaika kwa njia moja ama nyingine, ukiangalia kwenye TV wana matangazo kibao hayo yote yapo kwa manufaa yao kwanini na mwanamuziki asinufaike.”

Tuesday, April 29, 2014

FURSA: MAFUNZO YA KUPIGA ALA ZA MUZIKI KUANZA TENA MWEZI MEI

 Baadhi ya wanafunzi wakiwa kwenye mazoezi

Action Music Tanzania (AMTz) inatangaza fursa kwa watu wote kujiunga na mafunzo ya kupiga ala za muziki yanayoanza tarehe 3/5/2014, lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wanamuziki wa kupiga ala na kufanya maonesho kwa weledi na utaalamu zaidi.
Baadhi ya wanafunzi wakiwa darasani

Mafunzo yanayotolewa ni pamoja na upigaji wa ala za muziki zikiwemo gita, kinanda, tarumbeta, saxophone, konga, drum set, na upigaji wa ngoma za asili. Pia yatatolewa mafunzo ya ‘body percussion’ yaani matumizi ya mwili katika kutengeneza midundo ya muziki.

Mafunzo hayo yanafanyika kwenye ofisi za AMTZ zilizopo maeneo ya Mwenge mtaa wa Umoja, nyuma ya magorofa ya jeshi na kwenye Idara ya Sanaa na Sanaa za Maonesho Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo ili kujiunga na mafunzo haya wasiliana nao kwa simu namba 0686928828/0653075791 ili kupata fomu za kujiunga na mafunzo.

Monday, March 3, 2014

ONESHO LA WAPIGA ALA/VYOMBO VYA MUZIKI KUFANYIKA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM SIKU YA IJUMAA

Action Music Tanzania inayofuraha ya kukualika kuhudhuria onesho la muziki litakalofanyika siku ya Ijumaa ya tarehe saba mwezi wa tatu (07.03.2014) kwenye idara ya sanaa na sanaa za maonesho (FPA) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuanzia saa kumi na mbili na nusu jioni hadi saa mbili usiku (12:30-2:00), Kiingilio ni bure.
Onesho hilo limeandaliwa na AMTZ litawahusisha wanamuziki kutoka kwenye taasisi mbalimbali ambao wameshiriki mafunzo maalumu ya muziki kwa muda wa wiki mbili ambayo yamefanyika kwenye Idara ya Sanaa na Sanaa za Maonesho ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (FPA), kuanzia Februari 24 mwaka huu. Pia wakati wa onesho kutakuwa na zoezi la kuchangia mfuko wa AMTZ ambapo wageni wataombwa kuchangia kiasi chochote cha fedha ili kuijengea uwezo asasi wa kuendelea kutoa mafunzo ya namna hiyo kwa watu wengine.
AMTZ ni asasi isiyo ya kiserikali inayoundwa na walimu wa muziki kutoka katika taasisi mbalimbali za elimu ya muziki nchini na imesajiliwa na BASATA na kupata kibali cha kutoa mafunzo ya muziki ya muda mfupi. AMTZ imekuwa ikitoa mafunzo ya muziki kwa wanamuziki wa aina zote kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuandaa, kucheza na kufundisha muziki kwa kutumia mbinu mpya na za kitaalamu ili kuambukiza elimu ya muziki kwa wanamuziki wengine na hatimaye kuboresha ustawi wa muziki kwa ujumla wake nchini.
Kufika kwako katika onesho hilo utakuwa ni mchango mkubwa sana kwa wanamuziki wetu, asasi yetu na muziki kwa ujumla wake. Natanguliza shukran zangu za dhati na karibu sana

Contact:
Mandolin Kahindi
Executive Secretary
Action Music Tanzania